Hujafa hujaumbika, miaka 29 iliyopita kijana aliyezaliwa na jinsia mbili nchini Kenya Ruth Wangui amebadili jinsia yake na sasa ni mwanamume anayefahamika kama Ryan Muiruri.
Ni mojawapo ya watoto wengi wanaozaliwa duniani kila mwaka walio na umbo lisiloweza kufafanuliwa kuwa ni mwanamke au mwanamume kwa wakati huo.
Kulingana na Ryan, alipozaliwa, mamake na mkunga waliamua kumpatia jinsia ya kike kwani walimuona kuwa na maumbile ya mtoto msichana.
Uamuzi ambao haukumpatia amani katika miaka itakayofuata
Baadhi ya watu wanaozaliwa na jinsia mbili, wanataka kutofautishwa na wapenzi wa jinsia moja, kwani hali zao wanaeleza ni kuhusu jinsia wala sio sifa za uume au uke.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, kuna aina 42 tofauti ya watu wenye jinsia mbili ulimwenguni. Ijapokuwa hakuna takwimu zilizokusanywa kuhusu hili, wataalamu wanasema kuwa, kwa kila watoto elfu 20 wanaozaliwa, mmoja ana jinsia mbili.
'Mimi sikujua kwamba niko tofauti na watoto wengine wakike, niligundua hilo nilipokuwa na umri wa miaka mitano nilipokuwa nikicheza na wenzangu' Ryan amesema.
'Nilikuwa nikicheza wa wenzangu na shangazi yangu ambaye tuko rika moja, na baada ya muda nilianza kupigana na mwenzangu hapo ndipo wakagundua kwamba mimi sio mtoto msichana kamili kama walivyodhania, walinivua nguo na hapo ndipo niliweza kubaini kwamba ni kweli mimi niko tofauti, niligundua niko na sehemu nyengine ambazo wasichana wengine hawana.' Ryan aliongezea.
Anaeleza kwamba watu wenye jinsia mbili hubaguliwa, wengi hukosa kueleweka, na mara nyingi hutizamwa kama watu wenye laana.
Ryan ambaye sasa ni mwanaharakati na muasisi wa chama cha watu wenye jinsia mbili, anasema hali hii ya kuwa na jinsia mbili iliathiri maisha yake.
'Nilikuwa sina raha na hata marafiki zangu walinifanyia utani wakisema mimi huwa sitabasamu, lakini ni kwa sababu sijakutana na kitu chochote ambacho kimenifurahisha maishani mwangu.'
'Tangu kisa hicho cha watoto kugundua kwamba mimi sio msichana kamili walienda shuleni na kutangaza siri yangu. Wakati nilipokuwa ninakwenda haja watoto walikuwa wakinifuata kunitazama iwapo mimi hujisaidia kama kijana au huchuchumaa kama msichana, na maisha shuleni yalizidi kuwa magumu sana kwangu'.
Anaeleza hayo yalimfanya kutoroka shuleni na hata kujificha msituni lakini baada ya muda hilo likagunduliwa.
'Mamangu mzazi aligundua hilo kwani sikuwa na andika chochote katika vitabu vyangu'.
Mwaka wa 2004, ndipo aliianza safari ya kubadili jinsia yake kuwa mwanamume na anasema ulikuwa mwaka mgumu sana.
'Mahali nilipolelewa walizingatia dini sana, kwa sababu hata watoto wasichana hawakuruhusiwa kuvaa suruale ndefu ila marinda pekee'.
'Nilipopata muda wa kutoka nyumbani nilikuwa najifanya kijana na nikaanza kuvalia mavazi ya kakangu mdogo lakini niliporudi nyumbani ilinibidi nivae rinda na kujifanya mimi mi msichana kwani hivyo ndivyo wanavyonitambua
Ryan anakiri kwamba ni mtihani mkubwa na amewasihi wazazi iwapo watagundua kwamba wamejaliwa mtoto wenye utata au tofauti kidogo, ni vyema kutafuta ushauri kwa wakati muafaka na hata amewasihi wale ambao wana jinsia mbili kujitokeza watafute uhuru wa maisha yao.
Mtoto anazaliwa vipi na jinsia mbili?
Kulingana na Dkt. Andrew Remideus kutoka nchini Tanzania, hali hiyo hutokea katika utungishi wa mimba katika wiki ya tano au sita, ambapo kunatengenezwa jinsia kati ya kike na ya kiume na ndio hitalafu hutokea.
Na hitalafu hiyo husababisha utata wa kubaini jinsia kamili.
Kabla ya kufanya upasuaji wa kubadilisha mtu jinsia lazima daktari azingatie yafuatayo
•Mtu kufanyiwa vipimo
•Kubainisha viungo alivyonavyo vya uzazi
•Idadi ya homoni katika mwili wake
•hali ya mtu huyo anajihisi.
Hata hivyo, katika kipindi cha miaka michache iliyopita, watoto wenye jinsia mbili wamefanyiwa upasuaji na kuwa sawa. Upasuaji ambao hufanywa mara nyingi hurekebisha tu sehemu zenye matatizo kwa sababu sio lazima. Baadhi ya watu waliofanyiwa wanasema kuwa upasuaji huo ulikuwa na athari hasi maishani mwa watoto, kimwili na pia kiakili.
Ili kuwalinda watoto dhidi ya ukiukwaji huu, mataifa kama vile Malta, Ujerumani, Chile, Indonesia na Colombia yamepiga marufuku upasuaji wa aina hiyo kwa kuwa unafanywa bila ya kuzingatia maslahi ya mtoto.
Nchini kenya mchakato huo umeanza na jopokazi lililobuniwa na serikali ya Kenya kuchunguza sera na sheria zilizopo kuhusu watu wenye maumbile hayo, wamependekeza watambuliwe kama "jinsia ya tatu".
Jopo hilo pia linapendekeza jinsia ya watu hao ijumuishwe katika stakabadhi rasmi na vile vile washirikishwe katika sensa ya kuhesabu watu.
Ujerumani, ni taifa la kwanza duniani kuanzisha jinsia ya tatu kwa kuruhusu watoto wanaozaliwa na jinsia tatu kusajiliwa kuwa si wanaume au wanawake
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni