Serikali ya Tanzania imewataka raia wake kuipuuzia ripoti iliyovuja ya ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dkt Philip Mpango ametoa rai hiyo Bungeni hii leo alipokuwa akijibu hoja za upande wa upinzani kuhusu ukuaji wa uchumi.
"Hii niliyoshika ni ripoti ya IMF. Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) inakadiria uchumi wa Tanzania atakuwa kwa asilimia 6.8 na Benki ya Dunia inakadiria uchumi wetu utakua kwa asilimia 6.6 mwaka 2019. Hiyo taarifa unayoitumia ni ile iliyovuja."
Gazeti la Mwananchi limemnukuu Mpango akisema hayo alipokuwa anampa taarifa mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde aliyeinukuu ikionyesha uchumi wa Tanzania unakua kwa wastani wa asilimia nne.
Ripoti iliyovoja ya IMF inakadiria kuwa uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 4.4 mwaka 2019 toka asilimia 6.6 kwa mwaka uliopita.
Sakata la ripoti hiyo lilianza katikati ya mwezi Aprili ambapo IMF kupitia tovuti yake ilitoa taarifa kuwa imenyimwa ridhaa na Tanzania kuchapisha ripoti baada ya wataalamu wake kukamilisha tathmini yao nchini humo.
Matokeo ya ripoti hiyo hata hivyo yalivuja muda mfupi baadae na kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa kama Reuters na Bloomberg.
Jambo hilo lilizua gumzo kubwa ndani na nje ya Tanzania huku wapinzania wakiitaka serikali ya nchi hiyo kuvunja ukimya
Wiki moja baadae, Mpango alitoa ufafanuzi na kueleza kuwa serikali ya Tanzania haijazuia kuchapishwa kwa ripoti hiyo bali inaendelea na mazungumzo na IMF.
Mpango alidai kuwa kuna hoja za upande wa Tanzania ambazo hazikutiliwa maanani na wataalamu wa IMF.
Hata hivyo maelezo ya waziri huyo bado yaliendelea kukosolewa. Mtaalamu wa uchumi na kiongozi wa chama cha upinzani CUF Prof Ibrahim Lipumba aliiambia BBC Swahili kuwa, kwa utaratibu, mpaka inapofikia hatua ya kuchapishwa, majadiliano yanakuwa yameshafungwa.
"Kimsingi hakuna tena majadiliano, serikali yetu itoe tu ridhaa ili ripoti ichapishwe," alisema Lipumba.
Utaratibu wa IMF kuchapisha ripoti
Kupitia kifungu cha nne cha makubaliano, IMF inaruhusiwa kuchunguza uchumi , hali ya kifedha na sera ya ubadilishanaji wa fedha ya wanachama wake ili kuhakikisha kuwa mfumo wake wa kifedha unatekelezwa bila matatizo yoyote.
Hatua hiyo inashirikisha ziara ya maafisa wa IMF ya kila mwaka katika taifa hilo ili kuangazia data mbali na kufanya vikao na serikali pamoja na maafisa wa benki kuu.
Baadaye wanatoa ripoti kwa bodi kuu, ambayo hutoa maoni yake kwa serikali na kuchapisha ripoti hiyo katika tovuti yake baada ya kupata ruhusa kutoka kwa taifa hilo