Jumatano, 8 Mei 2019

Askofu Josephat Gwajima adai mkanda wa picha za ngono umetangenezwa na maadui zake


Askofu Josephat Gwajima


Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima nchini Tanzania, Josephat Gwajima amekanusha kuhusika na video ya ngono inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujib wa Gwajima, video hiyo imetengenezwa na aliowaita maadui zake ambao wanalenga 'kumnyamazisha'.
Akiongea na wanahabari kwenye viunga vya kanisa lake jijini Dar es Salaam, Gwajima amesema msimamo wake na maono juu ya nchi ndiyo yamefanya kusingiziwa kashfa hiyo.
"Watu wanafanya haya ili nikose sauti. Wanasema 'tumpige Gwajima ili anyamaze.'" amesema na kuongeza: "Hizi picha zinajaribu kunichafua, lakini hawawezi."
Gwajima, ambaye pia amekuwa pia kwa namna moja ama nyengine akihusishwa ama kuhusika na siasa amesema: "Uchaguzi unakuja mwaka kesho (2020) na wanajua nina nguvu, hawataki niwe na sauti yoyote.
Hata hivyo, Gwajima hakuwataja kwa majina hao aliowaita kuwa ni maadui zake.
Video hiyo inayodaiwa kuwa ni ya Gwajima inamuonesha akiwa faragha na mwanamke wakifanya tendo la ngono. Na mtu anayedhaniwa kuwa ni Gwajima ndiye alikuwa akiichukua video hiyo kwa kutumia kamera ya mbele ya kifaa ambacho hakionekani.
"Ni mwanaume gani ambaye mwenye akili zake timamu anayeweza kujirekodi wakati akifanya tendo la ndoa? Haingii akilini," amejitetea Gwajima na kuongeza, "Zile ni picha za kuunganisha. Wametumia picha yangu moja ya kifamilia nikiwa kifua wazi na kuunganisha na picha nyengine ili wanichafue."
"...mkono wa huyo mtu anayejichukua ile video ni mkubwa, ni mkono wa 'baunsa' sio huu mkono wangu mdogo."
Gwajima pia amewaambia wanahabari kuwa tayari amesharipoti tukio hilo kwa mamlaka husika na kusema anatumai mtu aliyechapisha picha hizo kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram atakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Askofu huyo aliambatana na viongozi wenzake wa kanisa lake pamoja na mkewe ambaye ameeleza kuwa ana imani na mumewe.
"...mimi ni jasiri kama Simba. Ukweli naufahamu. Mume wangu ninamfahamu na ninamwamini. Mungu akiwa upande wetu hakuna wa kutushinda," amesema Bi Gwajima.
Polisi waanza uchunguzi
Wakati huohuo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), wameanza uchunguzi juu ya video ya ngono 'inayomhusisha' Askofu Gwajima.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Jumatano, Mei 8, 2019 na Kamanda wa polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, imeeleza kuwa Mei 7,2019 kuna video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na watu wasiojulikana ikionyesha mtu anayefanana na mchungaji huyo akiwa na mwanamke asiyefahamika.
"Jeshi la Polisi Kanda Maalumu limeanza uchunguzi wa video hiyo mara moja na linapenda kuwapa taarifa wananchi (kuwa) Gwajima siyo mtuhumiwa, ni muathirika wa tukio hilo kwani tukio hilo linaweza kufanywa na mtu yeyote kwa nia ya kutaka kuharibu heshima yake kwa jamii na waumini," amesema Mambosasa.
Taarifa hiyo imesema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha kusambaza video hiyo kwa maelezo kuwa ni kosa la jinai na kuwataka waumini wa kanisa hilo kuwa watulivu kwani uchunguzi unaendelea ili kubaini aliyeisambaza na lengo la kufanya hivyo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni