Alhamisi, 9 Mei 2019

Mamia ya waombolezaji wamiminika kumuaga Mengi kijijini Machame leo

Maelfu ya waombolezaji wamehudhuria ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi.
Ibada hiyo imefanyika katika Kanisa Kuu la Usharika wa Moshi mjini wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Kutokana na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kuhudhuria ibada hiyo, polisi walilazimika kufunga barabara zote ambazo zinaelekea kwenye kanisa hilo.
Safu ya waombolezaji imeongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa na Spika wa Bunge la nchi hiyo Job Ndugai.
Mapema asubuhi saa tatu kanisa lilikuwa limejaa, na nje pia kulikuwa pamefurika. Baadhi ya waombolezaji walipata nafasi ya kuaga mwili ndani ya kanisa lakini ilifika mahala hatua hiyo ilisitishwa ili ibada na hotuba zitolewe.
Mwili ulitolewa kanisani kwa safari ya mwisho ya makaburini saa tisa na nusu. Na shughuli za mazishi zilikamilika saa 11 na nusu.

Familia yatoa neno

Familia
Image captionMke wa Mengi Jacquiline akiwa pamoja na watoto katika ibada ya mwisho ya mazishi ya mume wake
Mtoto mkubwa wa kiume wa marehemu Mengi, Abdiel, amesema kwa niaba ya familia wanashukuru na wameguswa na upendo waliooneshwa.
"Sisi kama familia tumeguswa sana na upendo ambao umeoneshwa kwa baba yetu. Mengi mazuri kuhusu mzee wetu mmeyasema. Mapenzi yao yamemgusa mzee wetu, hili ni uthibitisho kuwa muda na nguvu zake ambazo aliziwekeza kwa watu hawa hazikupotea bure. "
Abdiel amemzungumzia baba yake kuwa ni mtu ambaye alipenda kufanya mambo mengi na kujaribu na alikuwa na mipaka yake pia.
Mazishi ya Mfanyibiashara maarufu wa Tanzania Reginald Abraham Mengi
"Lakini hakuwa na mpaka kwenye kupambana na umasikini. Alikuwa na mtoto wa masikini lakini hakuna aliyeweza kumzuia kupambana na umasikini na kujikwamua. Pia hakukubali mpaka wa kuambiwa yeye kama mwekezaji mzawa basi hawezi fanya hili ama lile nchini. Hilo alilipinga kwa nguvu zote."
Jamaa waliyojawa na majonzi
Marehemu Mengi ameacha mjane, ambaye ni mlimbwende maarufu nchini humo Jacqueline Ntuyabaliwe na watoto wanne.
Umauti ulimfika usiku wa Jumatano ya wiki iliyopita jijini Dubai, Falme za Kiarabu ambapo alienda kwa ajili ya matibabu.

Mengi ni nani?

mENGIHaki miliki ya pichaIPP
Mengi alizaliwa wilayani Machame, Kilimanjaro, Tanzania mwaka 1942, akiwa mmoja wa watoto saba wa Bw Abhraham Mengi na Bi Ndeekyo Mengi.
"Familia yetu ilikuwa masikini sana, kila siku ilikuwa ni vita ya kupambana na umasikini. Tulimiliki sio zaidi ya ekari moja tukiishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng'ombe wachache na kuku. Ninaporudisha fikra na kutazama nyuma ni vigumu napatwa na ugumu wa kufikiri namna tulivyoweza kuishi katika hali ile," alipata kusema kwenye uhai wake.
Alianza safari yake kielimu shule katika shule ya msingi Kisereny Village Bush School, kisha akajiunga Nkuu District School, kisha Siha Middle School, na baadaye Old Moshi Secondary School. Kwa ufadhili wa Chama cha Ushirika kilichokuwa na nguvu ya kifedha ushawishi KNCU Mengi alisomeshwa masomo yake ya shahada ya kwanza ya uhasibu nchini Uingereza.
Baada ya masomo ughaibuni, Mengi alirudi Tanzania 1971 na kuajiriwa na kampuni ya Cooper and Lybrand Tanzania ( sasa PricewaterhouseCooper) mpaka mwaka 1989 alipoamua kujikita kwenye ujasiriamali.
Baada ya kuachana na ajira, Mengi aliiboresha kampuni yake ya Industrial Projects Promotion Limited na baadae kufahamika zaidi kama IPP Limited.
Kupitia IPP Limited Mengi alaianzinza kampuni mbalimbali na kufanya biashara kadha wa kadha kuanzia uzalishaji wa sabuni, soda, maji ya kunywa, madini, mafuta, gesi asilia na kilimo.
Hata hivyo, umaarufu mkubwa wa Mengi ni kutokana na kumiliki vyombo vya habari, kuanzia magazeti, vituo vya runinga na redio.
Mwaka 2014, jarida maarufu la masuala ya fedha la Forbes lilikadiria utajiri wa Mengi kuwa unafikia dola milioni 560.
    WAOMBOLEZAJI

    Hakuna maoni:

    Chapisha Maoni