Jumapili, 3 Februari 2019

Njombe: Mtoto mwengine apatikana msituni amefariki Tanzania

Mtoto mwengine alipatikana amefariki siku ya Ijumaa katika kijiji cha Matembwe wilayani Njombe huku visa vya vya mauaji kwa sababu ya matambiko na kutoweka kwa watoto vikiendelea kukumba eneo hilo.
Mwili wa mtoto huyo kulinga ana gazeti la The Citizen ulipatikana umetupwa katika msitu unaomilikiwa na wazazi wake mita chache kutoka nyumbani kwao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Matembwe ameambia gazeti la The Citizen kwamba alipokea ripoti za mtoto huyo aliyepotea siku ya Ijumaa mwendo wa saa kumi na mbili jioni.Bwana Malekela alisema kuwa aliarifu jamii yote ambaypo ilianza kumsaka karibu na nyumbani kwao pamoja na msitu mbali na magari yaliokuwa katika eneo hilo.
Mamake mtoto huyo aliwasili kutoka kazini na kugundua kwamba mtoto wake alikuwa ametoweka.
Babake mtoto huyo bado alikuwa kazini wakati huo wote.
Kulingana na The Citizen Tanzania, mtoto aliyepatikana amefariki alikuwa ameenda shambani kulima na mamake, lakini baadaye mamake alimshauri kurudi nyumbani ili kufanya kazi nyengine
Lakini mama huyo alipowasili hakumpata mwanawe.
''Ni wakati huo ndiposa alimwambia mumewe na utafutaji ukaanza'' , alisema mwenyekiti wa kijiji hicho.
Ni hadi mwendo wa saa nne usiku ndipo mtoto huyo alipatikana amefariki akiwa na majeraha shingoni.
Mtoto huyo alizikwa hapo Jumamosi.
DC wa Njombe Ruth Msafiri alisema kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na wakati mgumu kutokana na misururu ya utekaji nyara watoto na mauaji.
''Serikali tayari imetuma jopo kuchunguza mauaji hayo na tayari jopo hilo limeanza kazi yake'', alisema katika mazishi siku ya Jumamosi Wilayani Njombe.

Waganga wa tiba ya Kienyeji


Baadhi ya Waganga wa tiba za jadi wilayani Njombe wakijadiliana jambo baada ya mkututano na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani

Kisa hicho kinajiri huku Waganga wa tiba za jadi wilayani Njombe nchini Tanzania wakijitenga na tuhuma kuwa wanachochea mauaji ya watoto wilayani humo.
Kwa mujibu wa serikali, uchunguzi wa awali umebaini kuwa mauaji ya watoto sita wilayani humo yamechochewa na imani za kishirikina.
Watoto hao, wakiwemo watatu wa familia moja wenye umri chini ya miaka 10 wamepatikana wakiwa wamefariki katika mazingira ya kutatanisha huku baadhi ya viungo vyao kama macho, meno na sehemu za siri vikinyofolewa.
Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola Jumatano aliliambia Bunge kuwa imani za kishirikina zimechochea matukio hayo na tayari serikali ina majina ya wahusika wote.
Hata hivyo, katika kikao chao na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni wilayani Njombe waganga wa jadi wamesema wao si chanzo cha tatizo na kuitaka serikali ifanye uchunguzi zaidi
Kiongozi wa waganga wa tiba za jadi Antony Mwandulami amedai kuwa watu wamekuwa wakilipiziana visasi kwa mauaji na kusingiziwa waganga wa jadi.
"Kuna mambo mengi nyuma ya haya mauaji. Wapo ambao wanalipiziana visasi na hawaonekani lakini waganga wanalaumiwa kwa kusemwa kuwa wamepiga ramli chonganishi," amesema Mwandulami.

Hofu yatanda


Waziri Masauni (katikati) akiogoza moja ya vikao wilayani Njombe kujadili mikasa hiyo ya mauaji ya watoto
Image captionWaziri Masauni (katikati) akiogoza moja ya vikao wilayani Njombe kujadili mikasa hiyo ya mauaji ya watoto

Mwandishi wa BBC Swahili Leonard Mubali anaripoti kutoka Njombe kuwa hofu imetanda wilayani hapo kutokana na matukio hayo ya mauaji.
Wazazi wameongeza uangalifu kwa watoto zao, na kuna ambao wanaacha shughuli zao na kusindikiza watoto shule.
Akizungumzia hofu hiyo waziri Masauni amesema: "Nachotaka kuwahakikishia wananchi ni kuwa macho, masikio, roho na moyo wa serikali umehamia Njombe. Waamini kuwa serikali jambo hili tumelichulia uzito mkubwa… ni jukumu letu kuwalinda wananchi ambao ndio wameiweka serikali hii madarakani. Lazima tuhakikishe kuna ulinzi, na hilo lipo ndani ya uwezo wetu na wala hatuna msalie mtume."
Akizungumzia kikao na waganga wa jadi Masauni amesema lengo lilikuwa ni kuunganisha nguvu na kupata taarifa zaidi kutoka kwao hususan kuwataja wale ambao wanachochea uovu.
Msafara wa mazishi ya watoto watatu wa familia moja waliokumbwa na mkasa huo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni