SAKATA la kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdude Nyagawa limetua bungeni ambapo sasa, Bunge limetaka maelezo kujua alipo. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).
Bunge limeiagiza serikali kufuatilia taarifa za kada huyo baada ya kutekwa na watu wasiojulikana na kisha kutoweka naye. Habari za kutekwa kwa Dude zimeendelea kusambaa katika mitandao ya kijamii zikihoji alipo Mdude.
Wito huo umetolewa leo tarehe 6 Mei 2019 bungeni jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge baada ya Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa kutoa hoja ya kuahirisha kikao kwa ajili ya kujadili sakata hilo.
Awali Chenge aliitaka serikali itoe maelezo ili wananchi wajue hali ilivyo, kwa kuwa suala hilo linahusu uhai wa binadamu.
Akifafanua kuhusu sakata hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema, Jeshi la Polisi limeanza kufanya uchunguzi wa tukio la kupotea kwa Mdude tangu tarehe 5 Mei 2019.
Mhandisi Masauni amewataka Watanzania kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola utakaowezesha kupatikana kwa Mdude.
Mdude anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana tangu tarehe 4 Mei 2019, akiwa ofisini kwake Mbozi Mkoa wa Songwe
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni